Friday, January 8, 2016


Mwahima taabani baada ya kutangaza kujiunga na Jubilee

Mbunge wa Likoni Mwalimu Masoud Mwahima katika mkutano wa hadhara eneo la Likoni hapo awali. Amejipata matatani baada ya kusema kuwa anakihama chama cha ODM


MOMBASA,Kenya:Siku moja tu baada ya Mbunge wa Likoni Mwalimu Masoud Mwahima kutangaza kukihama chama cha ODM na kujiunga na chama kipya cha Jubilee Party, sasa wakereketwa wa kisiasa katika chama cha ODM wamemtaka kujiuzulu rasmi katika chama hicho.
Wakizigumza mjini Mombasa ya siku ya Alhamisi, wakereketwa hao walisema kuwa mbunge huyo kutangaza kukihama chama cha ODM inaonyesha wazi sio mfuasi rasmi wa chama hicho, na anafaa kutangaza kujiuzulu kama mbunge wa Likoni.
Wamesema kuwa uhusiano wa mbunge huyo na chama cha Jubilee ni maswala yake binafsi, na wala sio kwa malengo ya kuwasaidia wakazi wa eneo la Likoni na sharti afuate sheria za chama na kujihuzulu ili kufanyika kwa uchaguzi mdogo.
"Tunataka kumuwona Mwahima akiwa amejiuzulu ikiwa yeye ametanga kuhama ODM chini ya mrengo wa Cord na kujiunga na JAP ili tuanze kujiandaa na uchaguzi mdogo kwa sababu alichaguliwa na ODM, na kama amehama, basi kiti hicho cha ubunge eneo la Likoni hakina mtu," alisema Mohammed Abdallah, mmoja wa wakereketwa hao wa kisiasa.
Aidha, wamesema kuwa iwapo hatachukua jukumu la kujiuzulu, basi watamshinikiza kinara wa chama hicho Raila Odinga kumfurusha katika chama.
Haya yamejiri baada ya Mbunge huyo wa Likoni kutangaza kujiunga na chama kipya cha Jubilee kama njia mojawapo ya kutoa shukran kwa Rais Uhuru Kenyatta kutokana na juhudi zake za kuhakikisha kuwa maskwota katika shamba la Waitiki wanapata hati miliki za ardhi.

No comments:

Post a Comment